Translate

Translate

Sunday, 17 November 2013

HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIMU MAJALIWA(MB)NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI KATIKA UFUNGUZI WA MDAHALO WA KITAIFA WA DINI MBALIMBALI JUU YA USIMAMIZI WA RASILIMALI ZA UMMA TAREHE 30/05/2013 KATIKA UKUMBI WA BLUE PEAR-DAR ES SALAAM.

Ndugu mkurugezi wa baraza la dini mbalimbali za dini Tanzania;
Ndugu washirika wa maendeleo,
Ndugu maafisa wa serikali,        
Ndugu wawakilishi wa mashirika ya kiraia,
Ndugu wawakilishi kutoka kamati za PETS vijijini,
Ndugu wanahabari,
Wageni waalikwa,
Mabibi na mabwana.


Ndugu mkulugenzi;
Awali ya yote napenda nitumie nafasi hii kwanza kumshukuru mwenyezi Mungu ,kwa kutupa uzima,afya,nguvu ,na kibali cha kutuwezesha kukutana katika tukio hili muhimu .Nilishukuru pia baraza la dini mbalimbali nchini kwa kuhakikisha tukio hili muhimu linafanyika ili tuweze kuzungumzia masuala mbalimbali muhimu kuhusu mstabali wa maendeleo ya wananchi .Nashukuru pia kwa maamuzi yenu ya kuialika TAMISEMI katika shughuli hii kwani kwa kweli sisi ndio wenye dhamana kubwa na shughuli mbalimbali zinzzomlenga mwananchi wa kawaida .Ndio maana pamoja na majukumu tuliyo nayo BUNGENI kwa sasa lakini baada ya kupata mwaliko wenu tumefanya maamuzi ya kuweza kushiriki.Niwape pole pia washiriki mbalimbali waliotoka nje ya Dar es salaam kwa safari ndefu kutoka sehemu mbalimbali kuja hapa kushiriki kongamano hili muhimi.

Ndugu washiriki,
Napenda pia kutambua mchango na kutoa shukrani za dhati kwa wadau mbalimbali wamaendeleo na Taasisi mbalimbali kwa kuwezesha maandalizi ya shughuli hii kufanyika wakiwemo Baraza kuu la waislam Tanzania (BAKWATA,)jumuiya ya wakristo Tanzania(CCT),Baraza kuu la maaskofu katoliki  Tanzania (TEC),Kanisa la kiinjili la kilutheli Tanzania ,shirika la kikristu linalotoa huduma kwa wakimbizi Tanganyika(TCRS),Shirika la shughuli za maendeleo ya wanawake (WIA)pamoja na shirika la maendeleo la Norway(NCA).Mchango wenu ni mkubwa sana katika kusukuma gurudumu la MAENDELEO kwa wananchi na kwa Taifs kiujumla ,ninatambua kuwa na ushirka wa madhehebu ya dini katika kuchangia maendeleo nchini ni wa kihistoria.Ninapenda kuwapongeza zaidi kwa kuwa sasa sit u mnatukumbusha kuwajibika kupitia ibada mbalimbali bali pia mnashiriki katika kuelimisha jamii hata nje ya nyumba za ibada.Lakini kwa namna ya pekee zaidi napenda kuwapongeza kwa kuwa tunapata fursa ya kutafakari  juu ya wajibu wetu katika kuleta maendeleo endelevu.

Ndugu Mkurugenzi na Washiriki,
Mandeleo ya nchi yanawezekana endapo kila mmoja wetu mahali alipo atatizama wajibu wake kwa malengo na bila kusukumwa. Malengo ndio msingi mkubwa katika utendaji kazi.Kwa watumishi wa umma,pamoja na malengo mengine lengo kuu ni kuhakikisha kuwa wanawatumikia wananchi kwa kadri ya uwezo ,kujituma na kuwa waaminifu na wabunifu katika kutumia rasilimali zilizopo kwa ufanisi.Sote tunafahamu kuwa hakuna siku ambayo mtu atasema rasilimali zilizopo zinamtosheleza.lakini ni imani yangu kwamba,rasilimali ndogo zilizopo zikitumika vema zinaweza kuleta mabadiliko katika undendaji na baadae kuleta maaendeleo makubwa ya Taifa na wananchi kwa ujumla .Tangu kupata uhuru,serikali imekuwa ikifanya jitihada kuhusu kuhakikisha kuwa huduma bora zinawafikia wananchi.katika kufanikisha jambo hili,serikali imekuwa ikichukuwa hatua mbalimbali ikiwemo kuanzishwa kwa mpango wa uboreshaji wa serikali za mitaa ulioanza mwaka1998 ambao unalenga katika kupeleka madaraka kwa wananchi.Lengo la kuwa na maboresho ni kuhakikisha kuwa mamlaka za serikali za mitaa zinapewa uhuru wa kufanya maamuzi mbalimbali yahusuyo utoaji wa huduma kwa wananchi na kuwakilisha wananchi katika kujiletea Maendeleo na ustawi wao kwa ujumla.

Ndugu Mkurugenzi na Washiriki,
Kwa mujibu wa sharia ya serikali za mitaa sura ya 287,majukumu ya mamlaka za serikalia za mitaa ni pamoja na kudumisha amani,usalama ,utulivu na kutoa huduma bora za jamii na kiuchumi kwa wananchi ,kutekeleza shughuli za maendeleo pamoja na kupanga mipango ya maendeleo  endelevu.Aidha ,serikali inazingatia sana suala la ushirikishwaji wa wananchi katika mipango mbalimbali na utekelezaji wa wananchi katika mipango mbalimbali na utekelezaji wa shughuli za maendeleo.Hili linafanyika kwa kuzingatia Mpango wa fursa na vikwazo kwa Maendeleo (opportunities and obstacles to Development-O&OD).Mpango huu ulianzishwa na serikali sambamba na awamu ya pili ya program ya maboresho ya serikali za Mitaa(2002)kwa lengo la kusaidia jamii kuwa na uelewa mkubwa kuhusiana na umiliki wa mchakato wa maendeleo.Maelekezo ya kuwashirikisha wananchi katika shughuli za maendeleo ni ya lazima na maendeleo,sharia za fedha na hata katiba ya nchi.

Ndugu Mkurugenzi na washiriki,

Dhana na lengo  la kuwa na ufuatiliaji wa Matumizi ya Rasilimali za Umma kwa wananchi ni suala muhimu katika kuhakikisha rasilimali za Nchi zinatumika ipasavyo na hatimaye kuboresha huduma za jamii. Sote tunafahamu panapotokea kufujwa,kuharibiwa au kupotea kwa rasilimali za umma ambazo zilipangwa katika kuendeleza utoaji wa huduma kwa wananchi ,watu wote huathirika bila kujali dini,kabila rangi au eneo.Hivyo basi ili kuwa na uhakika wa matumizi mazuri ya rasilimali hizo,wananchi wote bila kujali tofauti zao za kiimani,hawana budi kuungana na kushirikiana pamoja katika ufuatiliaji wa mapato ya matumizi ya rasilimali zao.  Serikali inatambua na kuthamini  jitahada zinazofanywa na umoja wenu katika kutekeleza miradi ya kuijenga uwezo jamii kushiriki kufuatilia mapato na matumizi ya rasilimali za Umma katika wilaya takribani 25 Tanzania bara na visiwani.Nakiri kuwa yapo mafanikio kutokana na baadhi ya viongozi  wasiowajibika katika kuwa mafunzo  yenu yamewezesha kwa kiasi kikubwa kujenga uwajibikaji na kuboresha utolewaji wa taarifa na huduma katika maeneo mbalimbali.Azma ya serikali ni kuendelea kutoa ushirikiano nanyi wakati wote.

Ndugu Mkurugenzi na Washiriki,
Napenda nitumie fursa hii kutoa wito kwenu na jamii kwa jumla kuendelea kutoa ushirikiano kwa kuwabaini baadhi ya viongozi wa Halmashauri na vijiji wasio waaminifu wanaochangia kurudisha nyumba juhudi za kuleta maendeleo kwa kujinufaisha binafsi.Wapo  viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali za umma ikiwepo fedha za uendeshaji wa shule,huduma ya afya na pembejeo za kilimo lakini hawazifikishi katika maeneo husika.Ninapenda kuwatia moyo wanakamati za PETS pamoja na jamii kwa jumla kutokana tama pale wanapoona viongozi wachache wasio waadilifu wanatumia vibaya madaraka yao kujinufaisha binafsi. Jambo la msingi ni kuzingatia kuwa Nchi yetu inaongozwa kwa msingi ya sheria na Utawala bora. Hivyo tuepuke kujichukulia sheria mkononi au kufanya maamuzi yanayopaswa kuamuliwa  kisheria.Tumieni vyombo vinavyohusika na wahamasisheni  wananchi kuzingatia sheria  za Nchi  pale yanapojitokeza mapungufu kwa watendaji wa serikali na kwa jamii kwa ujumla.Vipo vyombo kama vile Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa –TAKUKURU na Jeshi la polisi,vitumieni  ili watuhumiwa washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.Viongozi wa vijiji na Halmashauri zote nchini  wanao wajibu wa kutoa ushirikiano wa dhati na wakati wote milango yetu ipo wazi kwa ajili ya kupokea ushauri na maoni yenu.

Ndugu washiriki,
Mwisho napenda kuwasisitiza juu ya umuhimu wa kuendelea na kuhamasisha umoja wa Taifa letu hasa katika kipindi hiki ambacho baadhi ya watu wameanza kupandikiza hisia za udini kwa wananchi kwa malengo binafsi.Nchi hii ni yetu sote na wote tunawajibika kuuenzi mshikamano ambao tumekuwa nao  katika kipindi chote tangu tulipopata uhuru.  Umoja na Amani tulivyonavyo ni msingi ambayo waasisi wa Taifa hili wametuachia kama urithi wa pekee kabisa.Navikikosekana vitu hivi dhana nzima ya maendeleo kwa wananchi wetu itakuwa ni ndoto.  Ninafahamu wote tunatambua changamoto zilizotokea katika nchi za jirani na jinsi ambavyo watoto na kina mama wasio na hatia walivyoathirika na wengine kupoteza maisha.Naomba wote kwa pamoja tuwe walinzi wa Amani na Utulivu tulio nao. Vitu hivi vikitoweka sisi sote bila kujali DINI,KABILA NA RANGI zetu tutapata madhara makubwa sana.
Nimalize kwa kuwatakia Mdahalo wenye mafanikio katika kukuza uwezo wa wananchi kufuatilia Matumizi ya Rasilimali za Umma kwa kuleta maendeleo kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Baada ya kusema haya machache napenda nitamke kuwa kongamano hili limefunguliwa rasmi.

                                           ASANTE SANA

No comments: